“SITAMWACHA binti yangu ateseke kama mimi
ninavyoteseka nikiwa katika siku zangu. Familia yangu inafanya nijihisi
najisi. Siruhusiwi kwenda jikoni, Siwezi kuingia hekaluni, Siwezi kukaa
na wengine,” ni sauti ya Bi. Manju Baluni (32).
Kuna hisia ya dhamira katika sauti ya Bi. Baluni. Alizungumza katika
Kijiji cha Uttarakhand, Jimbo lenye miinuko mingi kaskazini mwa India.
Nchini India, kuna ukimya kuhusu suala la afya ya wanawake, hususan
wawapo katika siku zao (hedhi).
Kuna mwiko uliojikita katika jamii hizi kuhusu suala la mwanamke
awapo katika hedhi: wanawake si wasafi, wachafu, wagonjwa na wakati
mwingine wamelaanika katika kipindi hicho. Watu wanaamini kuwa wanawake
wanaokuwa katika hedhi hawatakiwi kuoga na wana upungufu wa damu.
Uchunguzi wa hivi karibuni wa kampuni ya kutengeneza taulo maalum za
kujisitiri kina mama wanapokuwa katika hedhi umeonyesha kuwa asilimia
75% ya wanawake wanaoishi mijini bado wananua taulo hizo zikiwa
zimefungwa katika mifuko au gazeti ili kutoonyesha kilichomo ndani kwa
sababu ya aibu inayohusishwa na hedhi.
Na kamwe hawawaombi wanaume katika familia kuwanunulia taulo hizo
maalum. Nimekulia katika nyumba yenye wanawake wengi, lakini bado
hatuwezi kujadili kwa uwazi suala hili ambalo ni la kawaida.
Wasichana wanajifunza kuficha nguo zao wanazotumia wawapo kwenye hedhi
kwa wanaume baada ya kuzifua, anasema Rupa Jha. Mama yangu alitumia
mashuka makuu kuu na kuzificha katika sanduku, tayari kwa kutumiwa na
mabinti zake wanne.
Changamoto kubwa ni namna ya kukausha vipande hivyo vya nguo. Nina
kumbukumbu za kuhisi wasiwasi na mashaka juu ya mchakato mzima.
Nilifundishwa mbinu nadada zangu wakubwa – namna ya kuficha nguo zenye
madoa ya damu chini ya nguo nyingine bila ya mwanaume yeyote kugundua.
Hatukuthubutu kuziacha peupe kwenye jua ili zikauke kabisa.
Matokeo ni kwamba kamwe hazikukauka vizuri, ziliacha harufu ya
uvundo. Nguo hizo zisizo safi zilitumika tena na tena. Wanawake
wakisikiliza mwezeshaji kuhusu hali zao za usafi nchini India
Ukosefu wa maji ulifanya kazi ya ufuaji kuwa ngumu na isiyo na usafi.
Hali hiyo haijabadilika sana tangu wakati huo kwa wanawake wengi wa
Kihindi.
Uchunguzi mwingi uliofanyika siku za karibuni umeonyesha kuwa mila
hizi zimesababisha madhara makubwa ya kiafya. Imeripotiwa kuwa mmoja
kati ya wasichana watano nchini India anaacha masomo kutokana na kadhia
ya hedhi. Baadhi ya wasichana wanaacha kwenda shule wawapo katika
kipindi cha hedhi. Margdarshi mwenye umri wa miaka kumi na mitano
anaishi katika kijiji cha ndani cha Uttarakashi.
Anapenda kwenda shule japo inamaanisha safari ngumu akipita katika
eneo lenye vilima vikali. Kamwe hajawahi kukosa masomo, isipokuwa kwa
mwaka jana wakati ambapo nusura aache masomo baada ya kupata siku zake
kwa mara ya kwanza.
“Tatizo kubwa kuliko yote ilikuwa namna ya kukabiliana na hali hiyo.
Bado lipo. Najisikia kufedheheshwa, hasira na mchafu sana. Mwanzoni
niliacha kwenda shule.” Anataka kuwa daktari na anashangaa kwa nini
wavulana katika darasa lake wakati wa somo la elimu ya viumbe(baolojia)
wanacheka sana mwalimu anapoelezea njia ya hedhi.
“Nachukia. Natamani tungekuwa huru zaidi na kujisikia huru
tunapozungumzia suala hili. Hali hii inatokea kwa kila mwanamke kwa hiyo
kuna nini cha kuchekesha hapo?” Anshu Gupta, mwanzilishi wa shirika
lisilo la kiserikali, Goonj, anahisi kuwa tatizo hili limejikita katika
ukweli kwamba linahusishwa na wanawake.
Nchini India wanawake wanatumia taulo za kujihifadhi wakati wawapo
katika siku zao kwa kutumia nguo kuu kuu. “Si suala la wanawake pekee.
Ni suala la kibinadamu lakini tumelibagua. Baadhi yetu tunataka
kuondokana na utamaduni huu wa kuona aibu na kunyamaza. Tunahitaji
kuvunja utamaduni huu.”
Shirika hili linafanya kazi katika majimbo 21 kati ya 30. Shirika
hili pia linatengeneza taulo rahisi kutokana na nguo zilizochakatwa upya
ili kuwasaidia asilimia 70% ya wanawake wa India ambao hawawezi kupata
taulo salama na safi.
-BBC
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment