MWANAMKE mmoja amejilipua huku mshukiwa akiuwawa kwa
kupigwa risasi wakati wa operesheni ya polisi katika mtaa mmoja wa Saint
Denis jijini Paris. Tayari watu saba wamekamatwa kuhusiana na tukio la
mashambulizi. Polisi walishambulia nyumba moja mtaa wa Saint Denis
wakieleza kuwa mshukiwa anayedaiwa kupanga mashambulio ya kigaidi ya
Ijumaa ambayo yalisababisha vifo vya watu 129 mjini Paris.
Hatima ya mshukiwa huyo, Abdelhamid Abaaoud, ambaye awali alidhaniwa
kuwa nchini Syria bado haijulikani. Mkuu wa mashtaka Francois Molins
alisema habari za kijasusi zilikuwa zimedokeza kwamba yumo mjini Paris.
Wote waliofariki kwenye mashambulio hayo ya Ijumaa wametambuliwa,
serikali imesema.
Kundi la Islamic State (IS) lilisema lilihusika kwenye mashambulio
hayo. Operesheni hiyo mtaani Saint – Denis, ambako uwanja wa taifa wa
Stade de France unapatikana, ilianza mwendo wa saa kumi na dakika
ishirini saa za Ufaransa. Akiongea na wanahabari eneo la operesheni
baadaye, Bw. Molins alisema operesheni hiyo ilianzishwa baada ya udukuzi
wa simu na habari za kijasusi kudokeza kuwa Abaaoud, Mbelgiji mwenye
asili ya Morocco, huenda alikuwa nyumbani humo.
Mwanamashtaka huyo alisema mwanamke mmoja, ambaye kituo cha runinga
cha BFMTV cha Ufaransa kilisema alikuwa jamaa wa Abaaoud, alijipua baada
ya operesheni kuanza. Mshukiwa mwingine aliuawa na guruneti na risasi
za polisi, Bw Molins alisema.
Maofisa watano wa polisi kikosi maalum cha kupambana na ugaidi cha RAID
waliohusika kwenye operesheni hiyo walipata majeraha. Mbwa wa kikosi
hicho cha polisi kwa jina Diesel mwenye umri wa miaka saba pia aliuawa.
Wanaume watatu walikamatwa katika nyumba hiyo. Wengine wawili
walipatikana wakiwa wamejificha kwenye vifusi na wengine wawili, akiwemo
mwanamume mmoja aliyekuwa amekodisha nyumba hiyo walikamatwa. Hata
hivyo polisi hawakutoa majina ya waliokamatwa.
Watu 400 walijeruhiwa kwenye mashambulio yaliotokea Ijumaa, huku watu
221 kati yao bado wanatibiwa hospitalini, 57 kati yao wakiwa wamelazwa
kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi. Mataifa ya Ulaya yameendelea kuwa
katika hali ya tahadhari.
Jumanne, mechi ya kirafiki kati ya Ujerumani na Uholanzi ilifutiliwa
mbali muda mfupi kabla ya kuanza na ndege mbili za shirika la Air France
zilizokuwa zikielekea Paris kutoka Marekani zilibadilisha njia kutokana
na hatari za kiusalama. IS walisema walitekeleza mashambulio hayo
kulalamikia operesheni ya ndege za kijeshi za Ufaransa dhidi ya ngome
zake Syria, na kuahidi kushambulia zaidi. Rais wa Ufaransa Francois
Hollande alisema Jumatano kwamba IS wanatishia ulimwengu wote na kwamba
atatafuta “muungano mkubwa” wa kufanya kazi pamoja kuangamiza kabisa
wapiganaji hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment