Ads (728x90)

Tabs

Page

story_News-in-Brief
MWANANCHI
Wakati leo saa 10 jioni ndiyo muda wa mwisho uliopangwa kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania Urais ndani ya CHADEMA, hadi sasa hakuna mwanachama hata mmoja aliyejitokeza kuzichukua.
Hali hiyo inazidisha sintofahamu iliyougubika mchakato wa Urais ndani ya chama hicho na ndani ya UKAWA, kuwa huenda kuna ‘mtu wa nne’ anayesubiriwa kutoka nje ya chama hicho japo kuhusu Viongozi na Wabunge wa chama hicho walisema Edward Lowassa anakaribishwa mradi tu afuate kanuni na taratibu.
Suala la mgombea Urais wa UKAWA limeendelea kuteka mjadala wa kisiasa nchini huku Watanzania wakisubiri kufahamu nani atateuliwa kupambana na Mgombea wa  CCM, Dk. John Magufuli.
Katika Mkutano wake uliofanyika Mwanza Jumatano Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliwaomba Watanzania wavumilie wakati wanakamilisha taratibu za kumpata mgombea Urais.
Pia, ilielezwa kuwa chama hicho kilikuwa kinasubiri mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF unaofanyika leo, huku taarifa nyingine zikisema chama hicho kilikuwa hakijampata mgombea mwenza kutoka Zanzibar.
Ratiba ya kuchukua fomu za Urais na kurudisha ilikuwa inaonyesha ni leo na hakukuwa na dalili zinazoonesha watu kujitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema kuna marekebisho yamefanyika katika tarehe hiyo ya mwisho kurejesha fomu ambayo yatatangazwa ndani ya siku mbili au tatu ambayo yalilenga kupisha mchakato wa kura za maoni, baadae chama hicho kilitoa taarifa ya kusogeza mbele tarehe ya kurudisha fomu hadi Julai 31, 2015 saa 10 jioni.
MWANANCHI
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam, unaendelea pamoja na kujitokeza kasoro kadhaa, ikiwa na pamoja na baadhi ya watu kutumia mbinu mbalimbali ili kukwepa foleni.
Katika Kituo cha Bwawani Shule, Mtoni Kijichi, wanawake wawili waliojifanya wajawazito walibainika kufanya udanganyifu huo huku mmoja akiwa tayari amejiandikisha.
Hata hivyo, mmoja wa majirani ambaye anawafahamu, alidokeza kuwa anawafahamu wasichana hao na hawakuwa na wajawazito.
Mmoja alikuwa amekwishajiandikisha na aliwahi kuondoka mapema kabla ya mwenzake aliyekuja kwa staili hiyo na kushtukiwa.
Baada ya mzozo huo, aliondoka taratibu eneo la tukio ndipo baadhi ya watu walipoanza kumkimbiza kubaini iwapo  ni mjauzito au la, msichana huyo alitoa makaratasi aliyokuwa ameyafunga tumboni kama ujauzito na kuyatupa, huku akikimbia na kutokomea katika vichochoro vya Mitaa ya Mtoni Kijichi.
Mmoja wa wasimamizi wa kituo hicho, alisema kuwa hawana kawaida ya kuwakagua isipokuwa wanachoangalia ni hali za watu wakiwamo wajawazito, walemavu, wazee na wenye watoto wachanga.
Katika Vituo vingine baadhi ya wananchi walilazimika kuzipiga kavukavu kutokana na wengine kutaka kuwapita wenzao waliofika vituoni mapema.
NIPASHE
Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na  Daniel Yona jana wamekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yao ya kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Shilingi milioni tano.
Hukumu hiyo ilitolewa Julai 6 mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.
Baada ya hukumu hiyo, jana Wakili wa Serikali, Timothy Vitalis alisema Mahakamani hapo kuwa waliwasilisha maombi ya kukata rufaa wakitaja upungufu wa aina tatu kwenye mwenendo wa kesi iliyopita kwamba hati ya mashtaka haikuwa sahihi.
Alitaja eneo la pili lililosababisha kukata rufaa kuwa ni ushahidi wa Jamhuri haukuwa na uzito wa kuwatia hatiani na pia adhabu iliyotolewa ilikuwa ni kubwa.
Katika rufaa hiyo, Jaji wa Mahakama hiyo, Salvatory Bongole aliieleza Mahakama kuwa hataweza kuendelea na kesi hiyo kwa sababu mmoja wa waliokata rufaa anafahamiana naye.
Kesi hiyo itasikilizwa Julai 31 mwaka huu kwa sababu anayetarajia kuiendesha atatoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza mwaka 2008 wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya Uingereza.
JAMBO LEO
Wakati operesheni ikiendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wa mtandao wa watu waliovamia Kituo cha Polisi Stakishari kilichopo Ukonga Dar es Salaam, baadhi ya watuhumiwa wametoa siri nzito za kwa nini vituo vya polisi vinavamiwa na kuporwa silaha.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Askari waliopo kwenye operesheni inayofanywa Wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani zinaeleza kuwa baadhi ya watuhumiwa wamesema kwamba wanavamia vituo vya polisi ili kukusanya silaha ambazo zitawapa nguvu ya kugeuza utawala nchini ili uwe wa itikadi ya dini yao na wanavamia Vituo hivyo kwa ajili ya kuongeza idadi ya silaha katika himaya yao.
Gazeti la Jambo Leo limeandika kuwa watu hao wana mtandao nchi nzima na kwamba kutokana na imani yao ni ngumu kuwabadilisha msimamo wao hata wanapokuwa mbele ya vyombo vya dola.
Mwanajeshi mmoja ambaye aliongea na mwandishi wa habari wa Gazeti hilo alisema operesheni kama hizo amezifanya mara nyingi na hivi karibuni waliwakamata watuhumiwa wengine kama hao Morogoro nao walisema lengo lao ni kutaka kubadilisha utawala uwe wa itikadi ya imani ya dini yao.
Mtuhumiwa mmoja alipoulizwa kwa utani kwa nini hawaendi kuvamia maghala ya silaha Jeshini kama kweli wanataka kusimika serikali yao, alisema wameanza kukusanya silaha kwa vile ni wachache na kingine kinachowakwamisha ni jinsi ya kuingiza silaha ndiyo maana wanakusanya bunduki za ndani.
Uchunguzi unaonesha baadhi ya vijana wanatuhumiwa kuwa ndani ya mtandao huo na huwa wanatumiwa bila ya wao kuelewa undani jambo linalofanyika ili kuepuka siri kuvuja.
HABARI LEO
Familia ya Luciano Chole, mkewe na mwanawe, wameuawa kinyama baada ya vijana watatu kuwakamata na kuwapiga mapanga na marungu na miili yao kuiteketeza kwa moto Sumbawanga.
Hukumu ya kesi hiyo imetolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Sumbawanga, Mwakipombe Sambo ambapo ushahidi uliotolewa Mahakamani ulieleza kuwa familia hiyo ilitendewa unyama huo Aprili 17, 2011 katika Kijiji cha Miombo, Kata ya Mtenga wilayani Nkasi.
Kwa mujibu wa ushahidi washitakiwa wa mauaji hayo, Shija Ndigila, Deus Kizipe na Galus Antony, wanadaiwa walifika nyumbani kwa Chole siku ya tukio wakiwa na ujumbe kwa mtoto wake, Jailos Silvanus.
Ilidaiwa kuwa vijana hao watatu, walimweleza Chole na mkewe kuwa kijana wao, Jailos alikuwa akihitajika kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho.
Baada ya kukubaliwa kuondoka na Jailos, wazazi hao waliamua kufuata vijana hao kwa kificho na kisha wakishuhudia kijana wao akishambuliwa kwa marungu na kucharangwa kwa mapanga mpaka akafa.
Imedaiwa kuwa baada ya kuuawa kwa Jailos, wauaji hao walibaini kuwa wazazi wa kijana huyo walikuwa wakishuhudia, ndipo walipowavamia na kuwaua kikatili kwa kuwacharanga kwa mapanga.
Wauaji hao imedaiwa waliamua kukusanya miili ya marehemu na kuifunika kwa nyasi miili yao na kuichoma moto. Mbali na kuteketeza miili hiyo, ilidaiwa kuwa wauaji hao baada ya kumaliza ukatili huo, walikwenda nyumbani kwa wanafamilia hao na kuiteketeza nyumba yao kwa moto kisha wakatokomea kusikojulikana.
Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Jaji Sambo aliwahukumu washitakiwa hao kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuua watu watatu wa familia moja.

Post a Comment