Kisukari ni mojawapo ya magonjwa ya mmeng’enyo ambayo
husababisha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sukari katika damu kwa muda mrefu.
Dalili kuu za ugonjwa huu ni kukojoa mara kwa mara isivyo kawaida, hususan
nyakati za usiku, kuhisi kiu ya maji, mwili kuchoka, kupungua uzito wa mwili na
misuli, kupata muwasho katika viungo vya uzazi, majeraha ya kujikata na kuumia
yanayopona taratibu na kutokuona vizuri kwa sababu ya ukavu wa
macho.
macho.
Kuna aina tatu za ugonjwa huu nazo ni kisukari aina ya 1,
kisukari aina ya 2, na kisukari wakati wa ujauzito.
Kisukari aina ya 1 ni ugonjwa ambao mwili hautengenezi homoni ya insulini. Ugonjwa huu
mtu huweza kuupata katika umri mdogo na pia mtu anaweza kuupata ugonjwa huu
hadi anapofikia umri wa miaka arobaini. Ni asilimia ndogo ya idadi ya watu
hupata ugonjwa huu wa kisukari aina ya 1.
Wagonjwa wenye kisukari aina ya 1 wanahitajika kutumia aina
ya insulini ya kuchoma kwa sindano kwa maisha yao yote. Na ni lazima wawe na
utaratibu wa kupima kiwango cha sukari katika damu mara kwa mara pamoja na kuzingatia
mlo maalum ili kuepuka kiwango cha juu cha sukari katika damu.
Kisukari aina ya2 ni ugonjwa ambao mwili wa mgonjwa
hautengenezi homoni ya insulini ya
kutosha kwa ajili ya kurekebisha sukari, au seli za mwili za mgonjwa zinakuwa
zimepungua au hazina hisia dhidi ya homoni ya insulini na kushindwa kuchukua
sukari kutoka katika damu ili iweze kumeng,enywa na kutengeneza nishati au
kuhifadhiwa mwilini (hujulikana pia kama usugu
wa insulini). Kadirio la 90% ya wagonjwa wa kisukari wana aina hii ya
ugonjwa.
Baadhi ya watu wanaweza kumudu aina hii ya 2 ya kisukari kwa kupunguza uzito, kula
mlo sahihi (healthy diet), kufanya
mazoezi pamoja na upimaji wa kiwango cha sukari katika damu.Mbali na mazoezi na
kuzingatia mlo sahihi, aina hii ya ugonjwa hutibiwa kwa kutumia dawa za vidonge
vya kumeza ambavyo husaidia ufanyaji kazi wa homoni ya insulini. Aina ya pili
ya kisukari isipotibiwa ugonjwa waweza kuendelea na kuwa sugu na hapo mgonjwa
huitaji kupewa homoni ya insulini.
Wale walio na uzito mkubwa au uzito mkubwa kupindukia(obesity), wako katika hatari ya kupata
ugonjwa wa kisukari aina ya 2 ukilinganisha na wale walio na uzito wa kawaida.
Watu walio na mkusanyiko wa mafuta mwilini, mafuta katika tumbo (kitambi) wako katika hatari ya kupata
ugonjwa.Kuwa na uzito mkubwa au uzito wa kupindukia husababisha mwili
kutengeneza kemikali zinazoathiri mishipa ya damu na moyo, pia huathiri mfumo
wa mmeng’enyo.
Kuwa na uzito mkubwa,au kutoshiriki kazi za kuupa mwili
mazoezi ya kutosha, pamoja na kula bila mpangilio kunaiweka miili yetu katika
hatari ya kupata aina hii ya 2 ya kisukari. Mfano unywaji wa vinjwaji baridi
vyenye sukari kama soda kila siku, unaongeza hatari hiyo. Wanasayansi wanaamini
kuwa athari ya sukari katika vinywaji baridi yaweza kuwa ya moja kwa moja,
zaidi ya kuongeza uzito wa mwili.
Katika utafiti mmoja huko nchini Uingereza, ulionyesha kuwa
wanaume wenye kiwango kidogo cha homoni ya testosterone walikuwa katika hatari
ya kupata aina ya 2 ya kisukari.
Aina ya 3 ni kisukari wakati wa ujauzito (kitaalam hujulikana kama gestational diabetes),ugonjwa huwaathiri wanawake wakati wa ujauzito.Katika kipindi cha ujauzito baadhi ya kinamama huwa na kiwango kikubwa cha sukari katika damu na kuifanya homoni ya insulini kushindwa kumudu sukari hiyo kuchukuliwa na seli za mwili na kupelekea kuendelea kuongezeka kwa kiwango cha sukari katika damu.
Uchunguzi hufanyika wakati wa ujauzito, na wagonjwa wengi wa
aina hii huweza kutibiwa kwa kufanya mazoezi pamoja na kuzingatia mlo sahihi.
Asilimia ndogo ya wagonjwa ambao njia ya awali ya kutibu itashindikana, kiwango
cha sukari hupunguzwa kwa kutumia dawa
za vidonge za kumeza. Na endapo kisukari hakitagundulika au hakitatibiwa wakati wa
ujauzito kutapelea matatizo wakati wa kujifungua.Mtoto anaweza kuwa mkubwa zaidi
ya kawaida na kumsababishia mama matatizo.
Watafiti waligundua kuwa, kina mama walao kiasi kikubwa cha mafuta yatokanayo wanyama na lehemu kabla ya ujauzito wanakuwa katika hatari ya kupata kisukari wakati wa ujauzito ukilinganisha na wakinama wanaokula kiwango kidogo cha mafuta ya wanyama na lehemu.
Matibabu.
Kisukari aina ya 1 ni
aina ambayo mtu huishi na ugonjwa kwa maisha yote na mpaka sasa hakuna tiba
inayojulikana kuondoa ugonjwa. Aina ya 2 ni ile ambayo huweza kudumu kwa maisha
yote, lakini mgonjwa anaweza kuondokana na dalili za ugonjwa kwa kutumia
dawa,mazoezi pamoja na mlo sahihi. Baadhi ya watu wameweza kumudu kuondokana na
dalili za ugonjwa bila kutumia dawa kwa aina hii ya 2, na hii imewezekana kwa
kutumia mazoezi,mlo sahihi na kudhibiti uzito wa mwili.
Wagonjwa wenye aina ya kwanza ya kisukari hutibiwa kiwango cha sukari katika damu kwa kutumia homoni ya insulini kwa njia ya kuchoma sindano, pamoja na mlo sahihi na mazoezi. Wagonjwa wenye aina ya 2 pili hutibiwa kwa dawa za vidonge lakini wakati mwingine hata homoni ya insulini hutumika.
Ni muhimu kiwango cha sukari katika damu kutokuwa juu isivyo
kawaida ili kuepuka madhara kwa mgonjwa. Yafuatayo ni madhara awezayo pata
mgonjwa endapo hatatibiwa kisukari.
- Matatizo ya moyo-kuziba kwa mishipa ya damu ya kwenye moyo na kupunguza mzunguko wa damu kwenye misuli ya moyo (ischemic heart diseases).
- Shinikizo la juu la damu-ni kawaida kwa watu wenye ugonjwa sugu wa kisukari na huweza kupelekea hatari ya kupata magonjwa ya figo,macho, shambulizi la moyo na kiharusi.
- Kuathirika afya ya akili-Ugonjwa wa kisukari usipotibiwa, mgonjwa anaweza kupata matatizo ya msongo wa mawaza,sononi , wasiwasi na hata magonjwa mengine ya akili.
- Magonjwa ya fizi-ugonjwa umekuwa ukiwashambulia zaidi wale wenye kisukari.
- Kupoteza uwezo wa kusikia.
- Magonjwa ya uambukizi ya ngozi.
- Matatizo ya miguu- vidonda visivyopona, miguu kuwaka moto(peripheral neuropathy).
- Matatizo ya macho.
- Matatizo ya tumbo.
- Mkusanyiko wa tindikali katika damu.
- Kuathirika kwa mishipa ya fahamu.
- Tatizo la nguvu za kiume.
Katika
nyakati hizi kuna ongezeko la wagonjwa wengi wanaougua maradhi ya kisukari
ukilinganisha na miaka ya nyuma. Hii inachangiwa na kubadilika kwa mfumo wa
maisha. Ni vyema basi kuhakikisha kuwa unaonana na wataalam wa afya mapema
endapo utapata dalili za ugonjwa huu ili kuudhibiti na kuepuka madhara
yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.
Post a Comment